Unapotaka kuuza gari lako, haishii tu kwenye makubaliano ya bei, kulipana na kupeana funguo. Ili mchakato wa mauzo uwe halali kisheria na salama kwa pande zote mbili, kuna nyaraka muhimu ambazo unapaswa kuwa nazo. Bila nyaraka hizi, unaweza kujikuta kwenye matatizo ya kisheria au kushindwa kumalizana rasmi na mnunuzi.
Hapa chini ni muhtasari wa nyaraka kuu unazohitaji kwa ajili ya kuuza gari lako kihalali Tanzania:
1. Kadi ya Usajili wa Gari (Registration Card/Logbook)
Hii ni nyaraka kuu inayothibitisha umiliki wa gari. Lazima iwe na jina lako kama mmiliki halali. Kama jina ni la mtu mwingine, lazima uonyeshe ushahidi wa uhamisho wa umiliki (transfer). Kadi hii hutolewa na mamlaka ya Mapatao Tanzania TRA kulingana na aina ya usajili. Na kwasasa mfumo wa IDRAS wa TRA unatoa kadi ya gari kidigitali ambapo mteja anaweza kuprintiwa na mwenye gari kadi na baada ya malipo kukamilika ni jukumu la aliyeuza gari kubadilisha umiliki kutoka kwake kwenda kwa Mnunuzi
Ni muhimu: Usimkabidhi mnunuzi kadi hii mpaka malipo yote yatakapokamilika.
2. Hati ya Mauziano (Sale Agreement)
Hii ni mkataba unaoandikwa kati yako na mnunuzi ukionyesha:
- Jina la muuzaji na mnunuzi
- Maelezo ya gari (aina, namba ya usajili, namba ya chassis, Rangi)
- Bei ya mauzo
- Tarehe ya mauziano
- Sahihi za pande zote mbili
- Mashahidi wawili (inaweza kuwa mmoja upande wa muuzaji na mmoja upande wa mnunuzi)
Mkataba huu unaweza kuandaliwa na wakili au uandikwe kwa njia ya kawaida lakini ukazingatia maelezo yote muhimu.
3. Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au Leseni ya Udereva
Ili kuthibitisha utambulisho wako kama muuzaji, unatakiwa kuwasilisha nakala ya kitambulisho halali — iwe ni NIDA, leseni ya udereva au hati ya kusafiria (pasipoti) pamoja na nakala ya picha ya paspoti. Mnunuzi pia anapaswa kutoa utambulisho wake. Hii husaidia kuepuka udanganyifu au utapeli.
4. Nakala ya Bima ya Gari
Ingawa si lazima, ni vyema kuonyesha nakala ya bima iliyokuwapo wakati gari linauzwa. Kama bima bado inatumika, unaweza kumweleza mnunuzi aende kwa kampuni ya bima kufanya uhamisho wa jina. Hii ni muhimu kwa ajali au dharura zinazoweza kutokea kati ya kipindi cha uhamisho.
5. Stakabadhi ya Malipo (Optional lakini muhimu)
Ikiwa mnunuzi analipa kwa mkupuo au kwa awamu, ni busara kutoa stakabadhi (receipt) kwa kila malipo. Hii inalinda masilahi yako na kuweka kumbukumbu wazi.
Hitimisho
Kuuza gari si biashara ya mdomo tu — ni mchakato wa kisheria unaohitaji maandiko sahihi. Ukijipanga na nyaraka zote muhimu kama kadi ya gari, hati ya mauziano, kitambulisho, na stakabadhi za malipo, utaepuka migogoro na kulinda haki zako. Hakikisha pia mnunuzi anajua wajibu wake na hatua za kuhamisha umiliki, japo kwa sasa utaratibu wa kuhamisha umiliki unatakiwa kufanywa na aliyeuza gari. Uuzaji wa gari kwa kufuata taratibu za kisheria ni njia bora ya kumaliza biashara salama na kwa amani.