Kwa Nini Wanunuzi Wanakataa Gari Lako?

Loading

Kwa Nini Wanunuzi Wanakataa Gari Lako?

Kama umekuwa unauza gari kwa muda mrefu lakini wateja wanaangalia na kuondoka bila kununua, ni ishara kwamba kuna vitu vinavyowafukuza. Ili kuuza gari lako kwa haraka na kwa bei nzuri, ni muhimu kuelewa sababu hizi na kuzitatua mapema.

  1. Bei Kuwa kubwa

Sababu:
Watu wengi hufanya utafiti kabla ya kununua gari. Ikiwa bei yako iko juu kuliko magari mengine yenye sifa sawa, wengi hawatasumbuka hata kukupigia simu.

Suluhisho:
Fanya utafiti wa bei, linganisha magari yenye hali na mwaka kama wa kwako, kisha rekebisha bei yako kuwa ya ushindani. Unaweza pia kuongeza maelezo ya ziada (kama matairi mapya) ili kuliongezea thamani

2. Mwonekano Mbaya wa Gari

Sababu:
Gari chafu, lina mikwaruzo, au viti vilivyochakaa vinaweza kuwafanya wanunuzi wasifikirie hata kukutafuta hata kama gari ni zima na bei nafuu

Suluhisho:
Fanya usafi wa ndani na nje, matengenezo madogo madogo, piga polishi na safisha vizuri kabla ya kupiga picha au mteja kuja kukagua

3. Matatizo ya Kiufundi

Sababu:
Wateja huwa makini sana kuhusu hali ya injini, suspension, brakes na transmission na wengine huja na mafundi kabisa kwaajili ya kukagua gari na wamefika mbali zaidi wanakuja na vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa gari. Tatizo lolote la kiufundi linaweza kuwafanya walikatae gari.

Suluhisho:
Fanya service ndogo, kagua breki, tairi, na suspension. Kama kuna kasoro kubwa, sema ukweli lakini toa punguzo au ofa ya kushughulikia tatizo hilo kabla ya kuuza.

4. Historia Mbaya ya Gari

Sababu:
Gari lililowahi kupata ajali kubwa au ambalo lina historia mbaya ya matengenezo linaweza kukimbiwa na wanunuzi.

Suluhisho:
Kuwa mkweli kuhusu historia ya gari lakini eleza vizuri marekebisho yaliyofanyika na hali ya sasa ya gari. Ikiwezekana, toa ripoti ya ukaguzi wa gari kutoka kwa fundi wa kuaminika.

5. Maelezo yasiyojitosheleza kwenye Tangazo

Sababu:
Tangazo lisiloeleweka, lenye picha chache au lisilo na maelezo sahihi linaweza kuwafanya wanunuzi wasilichukulie kwa umakini.

Suluhisho:
Weka picha za kutosha, toa maelezo kamili kuhusu hali ya gari, mileage, mwaka wa kutengenezwa, bei na mawasiliano yako. Jibu maswali ya wanunuzi haraka na kwa ufasaha.

6. Kutokuwepo Tayari kwa Majadiliano ya Bei

Sababu:

Wateja wengi hutarajia kuomba punguzo la bei. Kukataa kabisa mazungumzo kunaweza kuwafanya waendelee kutafuta sehemu nyingine.

Suluhisho:
Weka nafasi ya mazungumzo kidogo (slightly negotiable). Unaweza kusema: “Bei ni ya maelewano kidogo kwa mnunuzi mwenye nia.”

7. Nyaraka Kutokuwepo au Kutokuwa Sawa

Sababu:
Kukosekana kwa kadi ya umiliki, na baadhi ya taarifa muhimu kunawafanya wateja wengi wahofie kutapeliwa au gharama za ziada

Suluhisho:
Hakikisha unakuwa na nyaraka zote muhimu. Kama kuna jambo halijakamilika, liweke sawa kabla ya kutangaza gari.

Hitimisho

Ili kufanikisha kuuza gari lako kwa haraka, ni muhimu kutambua mambo yanayowarudisha nyuma wateja na kuyatatua haraka. Andaa gari vizuri, weka bei ya ushindani, kuwa na nyaraka kamili na jibu maswali ya wanunuzi kwa uaminifu. Kwa kufanya hivi, utaongeza nafasi ya kupata mnunuzi haraka na kwa bei nzuri.