Unapofikia hatua ya kuuza gari lako, muuzaji hutarajia kuuza gari lake alipwe pesa yote na biashara iishie hapo lakini katika biashara kuna hali inayoweza kujitokeza na kama uuze kwa cash (malipo ya papo kwa papo) au kwa malipo ya awamu (installments). Kila njia ina faida na changamoto zake japokuwa moja ya mata. Hapa chini tumeangalia tofauti kubwa kati ya hizi njia mbili.
1. Uhakika wa Pesa (Cash) vs Hatari ya Malipo Kukwama (Awamu)
Cash:
Ukiuza gari kwa cash, unapata pesa yote mara moja. Hakuna kusubiri, hakuna masharti ya muda mrefu. Una uhuru wa kutumia pesa zako haraka.
Awamu:
Malipo ya awamu yanamaanisha mnunuzi atakulipa kidogo kidogo kwa muda fulani. Hii inamaanisha unaweza kusubiri miezi kadhaa mpaka upate hela yote na pengine ukachelewa kulipwa au usilipwe kabisa kiasi kilichobaki kama mteja sio muaminifu. Kuna hatari mnunuzi akashindwa kumaliza malipo na kukufanya upoteze muda na pesa.
2. Wateja Wanaovutiwa
Cash:
Wanunuzi wa cash mara nyingi huwa wachache lakini wako tayari kulipa haraka bila usumbufu wa mikataba ya muda mrefu.
Awamu:
Njia ya malipo ya awamu huvutia wanunuzi wengi zaidi, hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kulipa pesa yote mara moja. Hii inaweza kukupa wigo mpana wa wanunuzi lakini inakuweka kwenye hatari ya malipo kukwama.
3. Urahisi wa Mchakato
Cash:
Mchakato ni rahisi na wa haraka. Ukishakubaliana bei, mnunuzi analipa na unakabidhi gari pamoja na nyaraka zake na biashara inakuwa imeisha bila usumbufu wowote
Awamu:
Unahitaji kuweka makubaliano rasmi kwa maandishi. Lazima muelewane kuhusu kiasi cha awali (deposit), muda wa malipo, kiasi cha kila mwezi, na nini kifanyike kama mnunuzi akishindwa kumaliza malipo.
- Gharama za kufuatilia Madeni
Cash:
Ukiuza kwa cash, unamalizana kabisa na mnunuzi. Hakuna gharama za kufuatilia malipo, simu za kukumbushia, wala safari za kudai deni.
Awamu:
Utahitaji muda na nguvu kufuatilia malipo kila mwezi. Kuna usumbufu wa kumkumbusha mnunuzi, na kama atachelewa au kusitisha malipo, unaweza kuingia gharama za ziada za kisheria.
5. Hatari ya Kupoteza Gari au Pesa
Cash:
Hakuna hatari ya kupoteza pesa baada ya kuliuza. Mnunuzi analipa na anaondoka na gari.
Awamu:
Kama mnunuzi akishindwa kumalizia malipo, unaweza kujikuta katika mchakato wa kumnyanga gari, au unaweza kupoteza fedha zako na gari kabisa kama huna mkataba mzuri wa kisheria.=
6. Uhuru wa Kupanga Bei
Cash:
Kwa kawaida mnunuzi wa cash ataomba punguzo kwa sababu analipa mara moja.
Awamu:
Unaweza kuweka bei juu kidogo kama fidia ya hatari na muda wa kusubiri malipo. Wengi wanaokubali malipo ya awamu hufanya hivyo kwa gharama ya juu kidogo.
Hitimisho
Kama unataka pesa haraka, unataka uhakika wa malipo na bila usumbufu, kuuza gari kwa cash ni njia bora zaidi.
Lakini kama uko tayari kusubiri, uko na uhakika na mnunuzi na unataka kuvutia wanunuzi wengi zaidi, basi unaweza kufikiria kuuza kwa awamu, lakini kwa kuweka mkataba mzuri wa kisheria lakini pia kukubaliana na changamoto zozote zinazoweza kujitokeza
Mwisho wa siku, chagua njia inayoendana na mahitaji yako ya kifedha na kiwango chako cha kuvumilia hatari.