Kubageini bei ya gari si jambo rahisi, lakini ni jambo linalowezekana. Kwanza, kabisa Muuzaji yoyote wa gari anakuwa ameshapanga kiasi cha faida anachotaka kukipata katika biashara hio au bidhaa hiyo anayotaka kuiuza. Sasa linapokuja swala la kushushwa bei na mteja huwa ni swala gumu kidogo na hupelekea baadhi ya wauzaji kukataa kushusha bei kwakuona kuwa kiasi anachotaka kama faida kitakuwa kimepungua lakini pia baadhi ya wauzaji wapo tayari kupunguza kidogo katika faida yake ili kufanya uwepesi wa biashara kufanyika
- Fahamu Gharama Halisi na Faida Unayotaka:
Kabla ya kuanza mazungumzo kuhusiana na kuuza gari, ni muhimu kujua gharama halisi ya gari unaloliuza. Hii inajumuisha bei uliyonunulia, gharama za matengenezo au ukarabati wowote kama umefanya, na gharama nyingine zozote zilizohusika katika gari husika. Baada ya kujua gharama hizi, sasa unaongeza faida unayotaka japokuwa unashauriwa kuweka faida ambayo haitafanya bei kuwa juu zaidi kuliko uhalisia. Kwa mfano, unaweza kuamua kuwa unataka faida ya asilimia kadhaa au kiasi flani cha pesa. Kuwa jumla ya gharama hizi na faida unayotaka itakusaidia kuamua bei ya mwisho kabisa unayoweza kukubali bila kupoteza faida unayotaka.
- Onyesha Thamani ya Gari:
Badala ya kuzingatia bei pekee yake, Muonyeshe mteja thamani halisi ya gari lako. Mnunuzi akielewa kwanini gari lako umesema unaliuza kiasi flani au bei uliyoweka, atakuwa tayari kufanya biashara na wewe. Shawishi mteja wako kwa kumuelezea kwa undani sifa za gari hilo, matengenezo yoyote makubwa uliyoyafanya (ukiwa na risiti), vipengele vya ziada, na kwanini gari hilo ni bora kwake. Kwa mfano, unaweza kumwambia kuwa gari hili halina vipengele mfano nimeweka tairi mpya, unaona ndani lilivyosafi, halina shida ya injini wala giaboksi kuna redio nzuri nimekufungia lakini kama haitoshi unaona gari halijawahi kurudiwa rangi na limetunza vizuri ndio maana nimekutajia bei hio kwa maana huongezi chochote
- Kuwa na Ujasiri na Kutokuwa na Haraka:
Waswahili wana msemo usemao kuwa Mvumilivu hula mbivu, kwa hio Wakati wa kujadiliana bei,Muuzaji unapaswa kuwa na ujasiri katika bei unayoitaja. Ikiwa unaonekana wewe mwenyewe una mashaka na bei utakayoitaja au una haraka ya kuuza, mnunuzi anaweza kutumia hilo kukushusha bei zaidi. Ruhusu mteja atoe bei yake kwanza baada ya wewe kumtajia bei yako, na kisha jibu kwa ujasiri, ukieleza sababu za bei yako. Usikimbilie kukubali bei ya kwanza utakayotajiwa, hata kama inaonekana ina faida kwako bado. Mara nyingi, kujipa muda wa kufikiria kunaweza kusaidia kupata bei nzuri zaidi. Watoto wa mjini wanasema mtikise kwanza mteja uone
- Toa Chaguzi Nyingine:
Badala ya kushusha bei kwa haraka, unaweza kumpa uchaguzi mbadala ambao bado utakupa faida. Kwa mfano, badala ya kushusha bei ya gari, unaweza kutoa huduma ya ziada, kama vile “free oil change” baada ya ununuzi, au kumpa baadhi ya huduma bila malipo. Hii inaweza kumpa mnunuzi kufikiri kwamba amepata punguzo au faida, huku wewe ukiendelea kubakisha faida yako
- Tambua Bei ya Chini Kabisa:
Weka bei yako ya chini kabisa ambayo unajua kabisa kuwa hata nikiuza kwa bei hii bado faida yangu niliyoweka itakuwepo. Hii ni “limit” yako. Unapofikia bei hio, hupaswi kushuka tena chini zaidi. Ni bora kutokufanya hiyo biashara kuliko kuuza kwa hasara. Kumbuka, faida yako ndio kipaumbele chako. Ikiwa mnunuzi hawezi kufikia bei yako ya chini kabisa, basi ni bora kuendelea kutafuta wateja wengine
- Tumia Mbinu ya “Take It or Leave It” kwa Busara:
Muda mwingine unapoona hamfikii muafaka wa bei, baada ya majadiliano marefu, unaweza kutumia mbinu ya “take it or leave it.” Hii inapaswa kutumika kwa busara na kama suluhu ya mwisho tu, baada ya kujaribu mbinu nyingine zote. Hii ina maanisha kuwa huna nafasi ya kushusha bei tena na inaweza kumfanya mnunuzi atoe uamuzi wa mwisho.
Kwa kutumia njia hizi, unaweza kuzungumza bei kwa ufanisi, kuuza kwa faida, na kutengeneza hali ya “win-win” ambapo mnunuzi atahisi ameridhika na bei, na wewe kama muuzaji umefikia malengo yako. Kumbuka, lengo ni kuuza gari kwa faida huku ukijenga uhusiano mzuri na mteja wako.