Baada ya kuuza gari, kazi haishi pale tu unapokabidhi funguo na kupokea pesa. Ni muhimu sana kuhakikisha umebadili umiliki wa gari TRA, rasmi kutoka kwako kwenda kwa mnunuzi. Hii itakulinda dhidi ya matatizo ya kisheria au makosa ya baadaye yanayoweza kufanywa na mmiliki mpya. Hapa kuna hatua muhimu za kufuata:
1. Andaa Nyaraka Muhimu
Kabla ya kwenda TRA, hakikisha unakuwa na nyaraka zifuatazo:
- Kopi ya mkataba wa mauziano uliosainiwa na pande zote mbili.
- Kadi halisi ya Gari.
- Kitambulisho chako (NIDA au leseni ya udereva).
- Nakala ya kitambulisho cha mnunuzi.
Kuwa na nyaraka hizi kutarahisisha mchakato.
2. Tembelea Ofisi ya TRA
Uhamisho wa umiliki wa gari hufanyika kupitia TRA (Tanzania Revenue Authority).
Muuzaji na mnunuzi wanashauriwa kwenda pamoja ili kuthibitisha mchakato. TRA itahitaji:
- Fomu za uhamisho wa umiliki (zinapatikana TRA)
- Kadi halisi ya Gari
- Kitambulisho cha kila upande
- Risiti ya malipo ya ada ya uhamisho
Japokuwa kwa sasa TRA wamebadilisha mfumo wa usajili wa magari unaoitwa IDRAS ambao pamoja na kazi nyingine Muuzaji wa gari anawajibika kubadilisha umiliki mara baada ya kuuza kwa kuingia kwenye mfumo wa mlipakodi.
3. Lipa Ada ya Uhamisho
Kuna ada ndogo ya uhamisho wa umiliki ambayo inalipwa TRA. Ada hii inategemea aina na thamani ya gari.
Ushauri:
Ada hii mara nyingi hulipwa na mnunuzi, lakini ni vizuri kukubaliana mapema kabla ya kwenda TRA.
4. Hakiki Majina na Taarifa Zote
Kabla ya kukamilisha uhamisho, hakikisha majina ya mnunuzi na maelezo ya gari yameandikwa kwa usahihi kwenye mfumo wa TRA.
Hitilafu ndogo zinaweza kuleta shida kubwa baadaye.
5. Toa Nyaraka na Fomu kwa TRA
Baada ya kujaza fomu zote na kulipa ada, utawasilisha nyaraka TRA kwa muuzaji kuzipakia katika mfumo wake wa mlipakodi. Mchakato huu unaweza kuchukua siku moja hadi kadhaa kulingana na ofisi husika.
6. Pokea Uthibitisho wa Uhamisho
Baada ya uhamisho kukamilika, mnunuzi atapokea ownership card mpya yenye jina lake.
Ni muhimu uhakikishe mchakato umekamilika rasmi kabla ya kufuta jina lako kwenye kumbukumbu zako binafsi.
7. Futa Taarifa Zako Kwenye Bima na Road License
Baada ya uhamisho, wasiliana na kampuni ya bima na mamlaka za road license ili kuhakikisha huna tena majukumu yoyote ya kisheria kwa gari hilo.
Hitimisho
Kubadili umiliki wa gari ni hatua muhimu ya mwisho baada ya mauzo. Usipuuzie. Kwa kufuata hatua hizi, utalinda jina lako na kuepuka matatizo ya baadaye kama faini, ajali au makosa ya barabarani yanayoweza kufanywa na mmiliki mpya. Hakikisha kila kitu kinakuwa rasmi na kwa maandishi.